Friday, November 28, 2014

Mawe katika figo na athari zake kiafya

Ni tatizo ambalo linasumbua wengi lakini ambalo halifahamiki vizuri
Tumesikia habari mbalimbali zinazohusu tatizo hili na dhana mbalimbali ambazo zimekuwa zikijengwa.
Hata hivyo, baadhi ya watu hukumbwa na tatizo la kuwa na vijiwe katika figo na mfumo wa mkojo kwa jumla.
Mawe haya hutokana ama madini, chumvi au tindikali mbalimbali zinazotolewa mwilini.  Nchini Tanzania, baadhi ya wagonjwa hushtuka wakielezwa wana tatizo hili wakidhani labda wamerogwa, ila jambo la msingi watambue  hili ni tatizo la kiafya.
Aina za mawe katika figo
Aina za vijiwe katika figo ni pamoja na vijiwe vya calcium oxalate, vijiwe vya tindikali ya uriki (uric acid), vijiwe vya struvite (magnesium, ammonium na phosphate)
Sababu za vijiwe katika figo
Kwa kiasi kikubwa, vijiwe husababishwa na kukosekana kwa usawa wa maji, madini na tindikali mwilini, ambayo kitaalamu huitwa electrolyte imbalance.
Kuna magonjwa kadhaa ambayo husababisha kwa kiasi kikubwa kutokea kwa hali hii kama ugonjwa wa utindikali kwenye mirija ya figo, matatizo kwenye tezi za shingo, kukojoa chumvi chumvi za oxalate kupita kiasi na hali ya nyama za figo kuwa tepetepe.
Nani yupo hatarini?
Tatizo hili huwapata zaidi watu walio na historia ya familia zao kuwa na vijiwe kwenye figo, walio na umri kuanzia miaka 40 au zaidi,  ingawa tatizo hili linaweza kutokea katika umri wowote.
Pia, linaweza kuwapata wanaume zaidi kuliko wanawake, wana  upungufu wa maji mwilini, kwa lugha rahisi wale wasiopenda kunywa maji katika kiwango kinachoshauriwa.


Huwatokea wale wanaopendelea kula zaidi vyakula vyenye kiasi kikubwa cha protini, chumvi au/na sukari, walio na unene kupita kiasi, walio na magonjwa ya utumbo mkubwa  au waliowahi kufanyiwa upasuaji wa tumbo.
Dalili zake
Kujihisi kichefuchefu, kutapika, kukojoa mkojo uliochanganyika na damu. Wakati mwingine uwepo wa usaha katika mkojo  hasa iwapo kuna maambukizi ya bakteria, Maumivu wakati wa kukojoa.
 Mkojo kutoka kwa kiwango kidogo, mkojo hushindwa kupita katika mirija ya ureter na kusababisha figo kushindwa kutoa uchafu mwilini na kusababisha mlundikano wa uchafu kwenye damu hali inayojulikana kama postrenal azotemia, kushindwa kupita kwa mkojo husababisha pia kutanuka kwa sehemu tofauti za figo  na iwapo kutakuwa na maambukizi katika mkojo, mgonjwa anaweza kuhisi kuwa na homa
Vipimo na uchunguzi
Vipimo vinavyoweza kugundua tatizo hili na madhara yake ni pamoja na x-ray inayoonyesha mfumo mzima wa figo, mirija ya figo kwenda katika kibofu-ureta pamoja na kibofu cha mkojo.
Kipimo kingine huitwa intravenous pyelogram (IVP), vipimo vya CT-scan au MRI, ultrasound ya tumbo, kipimo cha mkojo na kuotesha, kipimo cha damu (FBP)
Matibabu yake
Matibabu ya vijiwe katika figo hutegemea na ukubwa wa vijiwe husika. Iwapo vijiwe vina ukubwa mdogo na dalili alizo nazo mgonjwa ni chache na hazimzuii kuendelea na kazi zake za kila siku, mgonjwa anashauriwa kunywa maji mengi kiasi cha lita 2 mpaka 3 kwa siku.
Hii husaidia kuviondoa vijiwe kutoka katika figo au njia ya mkojo na kutumia dawa za maumivu ili kupunguza maumivu iwapo yatatokea
Iwapo vijiwe ni vikubwa na dalili ni nyingi na zinamfanya mgonjwa ashindwe kuendelea na kazi zake za kila siku, mgonjwa anaweza kutibiwa kwa kutumia tiba zifuatazo:
Mawimbi mshtuko kutoka nje ya mwili  ili kuvunjavunja vijiwe na kisha vijiwe hivyo hutolewa nje kupitia kwenye mkojo, upasuaji na kisha kuvitoa vijiwe, kifaa maalumu kiitwacho ureteroscope, wakati mwingine upasuaji wa kuondoa tezi za parathyroid hufanyika.


Jinsi ya kuzuia tatizo hili
Mambo unayoweza kufanya kuzuia tatizo la vijiwe kwenye figo ni pamoja na kunywa maji mengi kwa siku na kuhakikisha unakojoa angalau lita 2.5 za mkojo kila siku.
Punguza utumiaji wa vyakula vyenye oxalate kama viazi vitamu, spinachi, soya, chai na chocolate, kula vyakula vyenye chumvi kidogo na punguza protini hasa itokanayo na nyama, hivyo tumia itakonayo na jamii ya kunde na maharage.
Potassium citrate husaidia kuongeza pH hivyo kuzuia wingi wa tindikali katika mwili. Kwa walio na tatizo la uzalishaji uliopitiliza wa tindikali ya uriki, wanaweza kushauriwa kutumia dawa aina ya Allopurinol.

 Maintained by an  ICT consultant and Director of Studies:  IFF YOU NEED HELP PLZ CALLA US VIA 0782 474941 0767 4749411 OR VIST www.kcckibaha.blogspot.com kcckimisha@gmail.com

No comments:

Post a Comment